MZEE CHILO ama Ahmed Ulotu, ni msanii mahiri wa filamu nchini,.
Huyu ni miongoni mwa wazee wachache, wanaofanya vizuri kwenye maigizo na filamu za kisasa nchini. Umaarufu wake umepaa maradufu tangu alipoibuka katika tamthiliya ya JUMBA LADHAHABU.
Ni kweli Jumba la Dhahabu, ndilo lililomtangaza zaidi, lakini Mzee Chilo ni mwigizaji kwa zaidi ya miaka 40.
Ndani ya tamthiliya hiyo, Mzee Chilo aliigiza kama mzee tajiri, mpole na mkimya, lakini `mafia’, mwenye kutumia fedha zake kufanya
maovu katika jamii na kulipa changamoto Jeshi la Polisi.
Kwa hakika, alifanikiwa kuwavuta watu wa rika zote, kutokana na umahiri wa kuigiza kama baba, anayewajali watoto wake, licha ya kuishi maisha ya anasa yanayoambatana na vitendo
vya uhalifu.
Amewahi kuigiza kama Mzee wa Kanisa anayekumbatia makasisi wenye kufanya maasi mengi, kwa kutumia nafasi zao hizo, ilhali yeye ni Mwislamu kwa dini.
Lakini, pia amewahi kuigiza kama muumini mwenye imani kali ya Kikristo, ambaye alifanyiwa ukatili wa kuibiwa mtoto na kulazimika kusamehe katika filamu ya 'Lost Twins'.
Enzi zake akiwa Azania Ni umahiri wake wa kuuvaa vyema uhusika, ndio uliomfanya, si tu
akubalike ndani ya jamii, bali hata miongoni mwa waigizaji na wachezaji filamu nyota nchini,
wanaopigana vikumbo kumshirikisha katika kazi zao.
Katika mazungumzo ya hivi karibuni yaliyozaa makala haya, Mzee Chilo anasema kwamba, fani hiyo iko katika damu yake. Anasema aliianza miaka mingi, tangu akiwa mwanafunzi katika Shule ya Sekondari Azania, jijini Dar es Salaam mwaka 1966, yaani miaka 44 iliyopita.
“Nilipokuwa kidato cha tatu niliteuliwa kuwa miongoni mwa wanafunzi ambao waliwakilisha Shule ya Azania katika mashindano ya sanaa ya maonesho ya jukwaani, maarufu kwa jina la Shakespeare, hapo ndipo nilifanikiwa kuvuta watu wengi ambao walisifu kipaji changu,” anasema.
Anasema kwamba baada ya kuibuka nyota katika mashindano hayo, aliteuliwa kushiriki Tamasha la Mackbeth, mchezo ambao ulikuwa miongoni mwa sanaa za maonesho ya majukwaani, iliyoandikwa na Shakespeare.
Tamasha hilo lilisafisha zaidi nyota yake, kwa kuwa alipata umaarufu mkubwa.
“Katika mashindano nilifanikiwa kuibuka mshindi wa pili, ambapo nafasi ya kwanza ilichukuliwa na mtoto wa Balozi wa Nigeria nchini Tanzania….Mtoto huyo alinishinda, kwa sababu ya Kiingereza ilikuwa lugha yake ya kwanza”, anasema.
Hata hivyo, ushindi huo ulimpa changamoto ya kujifunza lugha ya Kiingereza kwa bidii zaidi.
Pia, mashindano hayo yalimwongezea ujasiri wa kusimama mbele ya hadhara na kuigiza.
Kiu yake ya kusaka elimu Katika kuthibitisha kuwa alikuwa na kiu ya elimu, mwaka 1970 alijiunga na Chuo cha Utumishi wa Umma, kilichopo Magogoni jijini Dar es Salaam, ambapo alichukua kozi ya Utawala Bora na kutunukiwa cheti mwaka 1972.
Baada ya kuhitimu masomo, aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kisarawe katika kitengo cha kilimo.
Alifanya kazi hiyo kwa muda mfupi, kisha akajiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Akiwa jeshini, alitumia taaluma yake kufanya kazi za uongozi, jambo lililomwezesha kujenga uzoefu.
Baada ya kuhitimu mafunzo ya jeshi hilo, aliajiriwa katika Kampuni ya viatu ya Bora na baadaye aliamua kusoma, ambapo mwaka 1978 alijiunga na Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Madina, Saudi Arabia na kuhitimu Shahada ya Dini mwaka 1986.
Aliporejea nchini, alifanya kazi ya ualimu na kufundisha vipindi vya dini katika sekondari mbalimbali mkoani Kilimanjaro, ikiwemo Masama, Old Moshi, Weruweru, Kibosho, Umbwe na Mawenzi.
Mwaka 1995 aliajiriwa na Ubalozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, ambapo alifanya kazi mbalimbali katika kitengo cha utawala, ikiwa ni pamoja na kutafsiri nyaraka mbalimbali.
Alifanya kazi hiyo hadi mwaka 2002. Pia, alifanya kazi ya kuwaongoza mahujaji katika safari za Saudi Arabia, akiwa na Taasisi ya Haji Trust.
Juhudi za kutimiza ndoto ya uigizaji Mwaka 2002 aliamua kutimiza ndoto zake, kwa kujikita zaidi katika sanaa. Alianzia Taasisi ya Dunia Inc, iliyojishughulisha na utengenezaji wa matangazo na filamu na baadaye alitua Bahari Sanaa Group, ambako alikutana na walimu
wapya, ambao walimfundisha sanaa na miiko yake.
“Nilijifunza mengi na kwa mara ya kwanza nikaibuka ndani ya filamu inayoitwa 'Sumu ya Mapenzi' nikitumia jina la Ahmed,” anasema.
Kwa kuwa alijituma na kutumia vyema kipaji chake katika filamu ya kwanza, alianza kupata
umaarufu ; na mwaka 2006 akaanza kupata mikataba ya kufanya filamu mbalimbali, kama vile Filamu ya Utata, Tanzia na Simu ya kifo.
Umahiri katika filamu hizo, ulimkuna mmiliki wa kundi la Fukuto, Tuesday Kihangala, aliyemwalika na kumshirikisha katika tamthiliya ya Jumba la Dhahabu, jukumu lake kubwa kucheza nafasi ya mtu `mafia’.
Ili kuimudu nafasi hiyo, alipewa mafunzo mapya ya kujenga ujasiri, kuvaa uhusika pasipo kutetereka na kutumia kipaji chake kuonesha jamii, jinsi dunia inavyoweza kubadilika, ambapo hata baadhi ya matajiri huweza kujihusisha na vitendo vya uhalifu.
Mzee Chilo anasema kuwa baada vya kufanikiwa kuigiza vyema katika tamthiliya hiyo, aliamua kujikita katika filamu na maonesho ya jukwaani, ambapo alisaini mikataba
mbalimbali ya kushiriki katika filamu.
Katika uigizaji wake, amefanikiwa kushirikiana na wasanii mbalimbali, wakiwamo kina Vincent Kigosi `Ray’, Steven Kanumba `Kanumba’, Yvonne Cheyl `Monalisa’, Yusuph Mlela `Mlela’ na Charles Magali `Mzee Magali’.
Anasema tofauti na miaka ya nyuma, ambapo sanaa ya maonesho ya majukwaani ilipuuzwa,
hivi sasa imekuwa sehemu ya ajira ; na kwamba Watanzania wameanza kuvutiwa na sanaa za
nyumbani.
Na baada ya kuonja faida za filamu nchini, Mzee Chilo anakiri kuwa fani hiyo imemsaidia
kubadilisha kwa kiasi kikubwa maisha yake, kuanzia kipato hata umaarufu. Anasema kiu yake ni kuwa mwigizaji wa kimataifa, akilenga kushirikiana na wakali kutoka nchi zilizopiga hatua katika filamu duniani, kama India (Bollywood) na Marekani (Hollywood).
Anasema mikakati ya kutimiza ndoto yake, kwa kuanzia na India, mikakati inafanywa na mmiliki wa Kampuni ya Pilipili Entertainment, Sameer Srtvastiva