IMEKUWA furaha kwa wasanii wa kike pale wanapofanikiwa kupata mtoto au watoto ambapo wengi wao hupenda kuwahudumia watoto wao kwa asilimia kubwa.
Lengo ni kuweza kumpatia mtoto wake huduma anazostahili na kuweza kuwa karibu naye zaidi ingawa baadhi husema ni njia ya kujigamba kwa wengine.
Lakini kwa Msanii gwiji wa filamu Lucy Komba (31)amekuwa tofauti sana kwani yeye mtoto wake Strom Mbasha (2) anakosa muda mwingi wa kumhudumia kutokana na kutingwa na kazi hivyo mara nyingi anahudumiwa na wasichana wa kazi.
Wiki kati msanii huyo alizungumza kwa kirefu na mwandishi wa habari hii Minael Msuya kuhusu maisha yake nje ya sanaa.
Mwandishi: Wewe ni mama wa mtoto mmoja vipi, unamhudumiaje mtoto wako kabla ya kwenda kazini?
Lucy: Napenda kuwa mkweli siku zote, mimi naamka saa kumi na moja alfajiri hapo najiianda kwenda kazini, mwanangu anakuwa amelala bado. Hivyo sina ninachomuandalia.
Mwandishi: Kwa hiyo mtoto wako anahudumiwa na nani kama wewe unapoamka hufanyi shughuli yoyote tena ukizingatia bado mdogo?
Lucy: Pale nyumbani tuna wasichana wawili wa kazi, mmoja ni maalumu kwa kumhudumia mtoto na mwengine anafanya kazi zingine hivyo mwanangu anahudumiwa zaidi na wasichana wa kazi.
Mwandishi: Hujisikii vibaya mwanao anavyohudumiwa na wasichana hao,
Lucy: Nammis sana mwanangu na ninampenda zaidi hivyo jioni ninaporudi nyumbani na siku za mapumziko namhudumia muda wote, kwani napenda nimhudumie mwanandu wakati wote mwenyewe isipokuwa kazi zinanibana.
Mwandishi: Kwani unafanya shughuli gani zaidi mpaka ukose muda wa kumhudumia mwanao?
Lucy: Kama unavyoniona hapa ofisini, mimi ni Katibu Muhtasi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, muda wangu unabana sana hata baadhi ya kazi zangu za sanaa nashindwa kuzimudu.
Mwandishi: Una muda gani na kazi yako hii, vipi kuhusu familia yako inakutegemeaje?
Lucy: Muda mrefu kidogo nilianza hapa tangu mwaka 2003, kwenye familia kwa kweli nahudumia kawaida, mama yangu ndiye anayeitunza familia na kwa sasa bado niko chini ya himaya ya mama yangu siwezi kujigamba kwa chochote.
Mwandishi: Baba wa mtoto unaishi naye au vipi?
Lucy: Siishi na mume hata hivyo sina mpango wa kuishi naye kwa sasa labda baadaye sana.
Mwandishi: Matarajio yako baadaye ni yapi?
Lucy: Matarajio yangu ni kuwa msanii na mtunzi mahiri wa kimataifa ili niweze kuonyesha kipaji change na kuongeza kipato changu zaidi ili familia yangu hasa watoto wangu niweze kuwahudumia na kupata elimu bora.
Mwandishi: Tofauti na sanaa unamatarajio gani mengine?
Lucy: Mh! Mimi naipenda kazi yangu ya uigizaji zaidi hata hii niliyonayo ni kwa sababu tu nimesomea lakini nafikiria kuifanya sanaa kuwa kazi yangu pekee na nitafanya ndani na nje ya nchi. Naamini ndoto yangu itakuwa imetimia kwani hivi sasa sanaa inakuwa kwa kiwango kizuri na ninapenda kuibua vipaji vya wasanii wengi zaidi kama ilivyokuwa kwa wasanii mahiri na wanaokubalika Mzee Chilo, Iren Uwoya, Mkwere na wengine wengi.
Mwandishi: Nikitu gani ambacho usipokifanya kwa siku unaona kama hujafanya kazi siku hiyo?
Lucy: Dah! Nimelipenda swali lako maana umeigusa mboni ya jicho langu, napenda sana kuandika na kufikiria stori mpya kichwani na kuiandaa. Kila siku moja najitahidi niandike japo mistari kadhaa ya stori zangu ili niweze kuandaa filamu zangu na kazi yangu isidumae, nisipofanya hivyo kwangu sioni kama siku imeisha hii ni kwasababu naipenda kazi ya uigizaji kuliko vitu vingine vyote.
Mwandishi: Maishani mwako unampango wa kumiliki kitu gani ambacho unaona kitakuwa na manufaa kwako?
Lucy: Ninampango wa kumiliki nyumba ya ghorofa moja, tayari nimeanza ujenzi wa nyumba nyangu hiyo maeneo ya Bunju. Wasanii wengi wa bongo wanapenda ufahari wa magari mimi nahitaji kuwa na gari aina ya sports nafikiri litanisaidia kwa shughuli zangu.
Mwandishi: Je ungependa kuwa na watoto wangapi na mume atakayekuoa awe na vigezo gani?
Lucy: Napenda Mungu akinisaidia niwe na watoto watatu, pia mume wangu asiwe na tabia chafu, anizidi mimi urefu, awe mweupe, mtanashati, mpole na mwenye uwezo wa kutunza familia.