MARA nyingi watayarishaji wa filamu za Bongo hupenda kuwatumia wasanii wenye majina maarufu, kuliko kutafuta vipaji vipya ili kuvina nafasi.
Lakini hali hiyo ni tofauti kidogo kwa mwongozaji na mtayarishaji wa filamu, William John, maarufu kwa jina la Mtitu, ambaye ni Mkurugenzi wa 5 Effect ya jijini Dar es Salaam.
Awali alianza na filamu iliyojulikana kwa jina la Sandra ambapo aliwashirikisha wasanii waliokuwa wakivuma na michezo ya kuigiza kama Single Mtambalike na Haji Adam.
Mtayarishaji huyo ambaye anaamini kuwa ukiwa na hadithi nzuri inaweza kuwakilishwa na msanii yeyote mwenye sifa na vigezo vya kuigiza.
Wasanii aliowaibua na kuwa nyota hadi leo ni Aunt Ezekiel, Yusuph Mlela, Irene Uwoya na Mariam Ismail. Wasanii hao kwa sasa ni nyota na wanatesa katika tasnia ya filamu.
Aunty Ezekiel
Msanii huyu kwa mara ya kwanza kabisa alishiriki filamu iliyojulikana kwa jina la Miss Bongo, Mtitu anasema kuwa baada ya kuandaa filamu hiyo, alifanya usahili kwa wasanii mbalimbali lakini nafasi ya Miss ilisumbua hadi alipompata
Yusuph Mlela
Ni kijana aliyekuwa katika fani ya mavazi, lakini Mtitu alimwibua na kumfanya kuwa mmoja kati ya wasanii wanaotesa katika tasnia ya filamu, alipomshirikisha katika filamu ya Diversion Of Love.
Humo aliigiza nafasi ya msanii chipukizi na kuibuka mshindi katika Tuzo za Vinara kupitia filamu hiyo.
Irene Uwoya
Hana tofauti na Mlela kwani naye akitokea katika mambo ya urembo kama alivyokuwa Aunty Ezekiel, alipewa uhusika katika filamu ya Diversion Of Love na kufanya vizuri.
Mariamu Ismail
Ni msanii ambaye tayari anatikisa anga hizi za tasnia ya filamu baada ya kuibuliwa na Mtitu kwa kumshirikisha katika filamu ya Best Man, ambayo ameiigiza kwa umahiri mkubwa na kuwafunika baadhi ya nyota.
Mariam alimudu kuigiza na nyota wakubwa kama Cloud, Mlela na Hemed.