Herieth Makwetta
KUNA msemo unasema: "Kitanda usicholalia hujui hila yake". Kwa tafsiri, msemo huu una maana pana zaidi, na nimeamua kuutumia kama sehemu ya taswira ya uchambuzi wangu wa leo.
Kupitia msemo huu, maana yangu ni kwamba tuepuke utamaduni wa kutoa majibu mepesi kwa maswali magumu, lakini pia sawa na kusema tuepuke kutarajia makubwa bila kuwa na malengo.
Wakati wa mazishi ya msanii maarufu wa filamu, Steven Kanumba, Aprili 10 mwaka huu, akitoa salamu kwa niaba ya serikali, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi alisema, namnukuu: "Mwaka huu ni mwisho wasanii kuibiwa kazi zao".
Kama haitoshi, Waziri Nchimbi aliutaja Agosti kuwa ndiyo mwisho wa wizi huo uliodumu miaka chungu mzima.
Napata mashaka kidogo kama vita ya kupambana na wezi wa kazi za wasanii imeweza kudumu kwa miaka mingi kiasi hicho bila mafanikio, halafu leo ije imalizwe katika muda wa miezi mitatu tu.
Ikumbukwe kwamba, wasanii wamekuwa na kilio cha kuibiwa kazi zao kwa muda mrefu na mikakati mingi ilitangazwa kukabiliana na hali hiyo, lakini mpaka sasa hakuna la kujivunia.
Sasa tunapokuja na mikakati mipya ya kupambana na hali hii, ni lazima pia tuangalia nyuma ni kwa kiasi gani tuliweza kufainikiwa tulipoingia kwenye vita hiyo.
Bila kwanza kufanya tathmini ya kweli, ni vigumu kupata majibu ya kweli katika vita hii ambayo naamini kama dhumuni la dhati linawekwa mbele na wadau wakasapoti, bila shaka hakuna litakaloshindikana.
Sina nia ya kupaka rangi nyeusi juhudi za serikali katika kupambana na wizi huo, kwa maneno mengine niseme tu, naungana mkono jitihada zote zitakazochukuliwa kukomesha wizi huu.
Tatizo nilionalo mimi ni kwamba, tuna utamaduni wa kuingiza mambo ya siasa maeneo ambayo kimsingi hayastahili kabisa. Tusijenge porojo kwenye eneo linalohitaji utekelezaji wa vitendo.
Kama mdau wa burudani na wasanii, nafahamu kazi ni ngumu tena inayohitaji nguvu ya ziada katika kutetea kila jasho linalomvuja msanii. Usimamizi wa hali ya juu unahitajika.
Vita hii haitakuwa na mafanikio kwa serikali bila kuwapo na uwekezaji wa msikamano na umoja toka kwa wadau na wapenzi wa sanaa nchini wenye kiu ya kuona wasanii wanakombolewa.
Katika salamu zake, Nchimbi alisema Wizara yake ikishirikiana na Wizara ya Fedha, Wizara ya Kazi na Ajira na Shirikisho la Filamu nchini (TAFF), wameshakutana na kujadiliana namna ya kuzuia wizi huo.
Ifahamike kwamba siyo wa kuzuia wizi pekee yake, kwa vile katika hilo kuna sekta nyingi zinahusika kumkandamiza msanii na mojawapo ni media mbalimbali zinapokea kazi za wasanii na kuzitambulisha kwa jamii.
Kuna matamasha mengi yanafanyika nchini, lakini ukweli ni kwamba hakuna anayefuatilia na kubaini kama wasanii wanalipwa haki zao kama inavyostahili.
Waziri Nchimbi ajisumbue kidogo kwa kuwauliza wasanii wa muziki wa kizazi kipya wanalipwa kulingana na ukubwa wa maonyesho wanayofanya. Atapata jiwabu.
Lakini pia, wasanii wamekuwa wakitumika kutangaza matangazo mbalimbali, je wanapata kulinangana wanachotoa? Hakuna wizi katika hili? Haya ni mambo ya msingi kujiuliza.
Wanaotumia kompyuta kwa kusambaza na kuuza kazi za wasanii wanatoa malipo kwa wasanii? Wasambazaji wanafanya wanavyotaka katika kuuza kazi za wasanii, wanawasainisha mikata isiyokuwa na tija kwao.
Huu nao wizi wa kazi za wasanii, tena ni vigumu kuudhibiti. Kana kwamba haitoshi, wapo baadhi wanatengeneza kazi feki za wasanii na kuziuza bei rahisi.
Sheria iliyopo dhidi ya watu wanaokamatwa wakirudufu kazi za wasanii na kuziuza, haina meno na kwa muonekana wake imekuwa kama kichocheo cha kuendelea kuwapo kwa hali hiyo.
Eneo hili ni lazima lifanyiwe marekebisho, kwa maana ya nyongeza ya adhabu dhidi ya wezi hao ambao baadhi yao jamii imekuwa ikiwakumbatia na kuwafanya kama watu wema.
COSOTA chombo kilichobeba dhamana ya kusimamia ulinzi wa haki za wasanii nchini, kimeshindwa kufikia malengo yake. Hili halina ubishi, kwani hali ya kuibiwa wasanii imeendelea kuwapo.
Ukichunguza kwa makini ni takribani miaka mitano sasa COSOTA haina bodi, ilikuwa inapataje ruzuku? Audited reports zilikuwa zinapitishwa na nani?
COSOTA hukusanya fedha kwa niaba ya wasanii bila kuwa na Bodi, sasa ushahidi gani unaweza kuwekwa mbele ya jamii juu ya matumizi ya fedha hizo.
Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kuwa pato la sekta ya sanaa ya muziki peke yake linafika Sh78 Bilioni. Je, itakuwaje na sekta ya filamu ikijumuishwa hasa ukizingatia kuwa filamu za Tanzania zinauzwa sana ndani na nje ya nchi?
Nina hakika kama serikika ingekuwa makini katika hili, bila shaka ingekusanya mapato mengi ambayo yangeweza kutumika katika shughuli mbalimbali za ustawi wa jamii.
Lakini pia wasanii wangeweza kupata stahili zao ya malipo kutokana na kazi zao. Tumeona viongozi wakishiriki katika uzinduzi wa albamu mbalimbali za wasanii, hapa ukweli ni kwamba anayetangazwa siyo msanii ila msambazaji wa kazi ambaye hata kodi halipi?
Ni wajibu wa viongozi na watendaji wa Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo kuanza kupitia suala moja baada ya jingine ili kujiridhisha kwa kupata taaarifa kamilifu kuhusu sekta ya sanaa kabla ya kuanza kutekeleza kazi hii.
Habari hii ni kwa hisani ya gazeti la Mwananchi.