Wanafunzi watatu wa Chuo Kikuu cha Mainz cha Ujerumani, waliopata kushiriki katika filamu na vichekesho nchini, wanajiandaa kuondoka baada ya kumaliza utafiti wao kuhusu masuala mbalimbali ya sanaa za maigizo, utamaduni, mila na uandishi wa habari katika jamii ya Tanzania.
Katika utafiti wao ulioanza mapema Agosti, wanafunzi hao ambao wanazungumza Kiswahili bila ya shida, wameamua kuishi na watu wa kawaida, jambo ambalo linaonekana ni tofauti na wageni wengine ambao mara nyingi huishi kwenye mahoteli ya kifahari.
“Tunaishi na watu wa kawaida katika sehemu za uswahilini. Hatukai katika mahoteli ya kifahari kama wazungu wengine,” alisema mmoja wa wanafunzi hao, aliyejitambulisha kwa jina moja la Jorn, alipofanyiwa mahojiano.
Alisema yeye anafanya utafiti kuhusu Watanzania wanavyopokea mambo mbalimbali wanayoyaona kwenye tamthilia mbalimbali za kutoka nje ya nchi na za ndani kama 'Ze Comedy' — zinazorushwa kwenye runinga.
“Lengo langu hasa ni kujua, ni kitu gani kinawafanya Watanzania kuangalia vipindi hivi, na jinsi wanavyoishi kulingana na maisha wanayoyaona kwenye vipindi kama hivi,” alisema mtafiti huyo mwanafunzi.
Kama sehemu ya utafiti, alisema, mtafiti unalazimika kukaa pamoja na watu wa kawaida na kuangalia vipindi hivyo ili kujua ni masuala gani yanawafurahisha Watanzania katika vipindi hivvyo.
Mwanafunzi mwingine, aitwaye Marie, alisema anafurahishwa na ujuzi na utaalamu wa waigizaji wa Kitanzania katika vipindi mbalimbali vya maigizo vinavyorushwa kwenye televisheni ya ITV na EATV.
“Ni utaalamu wa viwango vya juu unaofanywa na waigizaji wa tamthilia hizi. Nimeshaongea na baadhi ya waigizaji hawa, na bado naendelea kuwahoji kama sehemu ya utafiti wangu,” alisema Marie.
Mwanafunzi mwengine, Jan, alisema wanachukua muda mwingi kuishi na watu wa kawaida uswahilini, kula vyakula vya watu wa kawaida, kupanda madaladala -- ili kujifunza kwa urahisi mila, tabia, utamaduni wa Watanzania na watu wa Afrika Mashariki kwa ujumla.
Jorn ameshiriki katika filamu mbalimbali za nchini zikiwemo za 'Zaidi ya Rafiki' na Tears on Valentine's Day', ambazo tayari ziko sokoni zikipatikana katika DVD na CD.
Baada ya utafiti wao, unaotarajia kumalizika mwezi huu, wanafunzi hao wanatarajia kuandika kitabu chenye kichwa “Utafiti wa Vyombo vya Habari Afrika Mashariki (Media Studies in Africa). Vijana hao wamewaomba Watanzania na watu wa Afrika Mashari kuwapa maoni yao kuhusu thamthilia za nje na za ndani, na masuala mengine kupitia.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment