FILAMU ya DNA iliyoripotiwa kutoka hivi karibuni kutoka kampuni ya SAM Enterprises ya jijini Dar es Salaam imebadilishwa jina na haitaitwa DNA tena bali kwa sasa itaitwa Hidden Truth, badiliko hilo limefuatiwa na ombi lilotoka kwa mtayarishaji mwingine William Mtitu kumuomba mtayarishaji wa filamu hii Seleman Mkangara.
“Filamu hii niliita DNA kulingana na kisa cha filamu yenyewe, sasa akatokea jamaa akidai na yeye ana filamu ambayo ipo tayari kutoka na ina jina kama la filamu yangu DNA kwa hiyo akaniomba nibadili jina hili na kuita jina lingine, sikuwa na jinsi maana hawa wenzetu wanategemea kuuza kwa majina sasa uking’ang’ani filamu yake ikifanya vibaya wewe ndio utaonekana tatizo, kwa filamu hii sasa itaitwa Hidden Truth”
Alisema Mkangara.
Filamu hiyo ambayo imeigizwa kwa ustadi na mwanadada nyota na mshindi wa tuzo za Risasi mwaka 2005/ 2006 Riyama Ally imetabiriwa kuwa ni moto wa kuotea mbali, hata mtayarishaji wa filamu hii alisema kuwa kwa sababu ya uzuri wa filamu hii ndio maana hata alivyoambiwa na mtayarishaji mwenzake abadili jina alifanya hivyo haraka kwani anaamini kuwa haitaharibu chochote.
Binafsi nilikuwa sielewi kama majina nayo yanakuwa issue kubwa hivyo, suala la kugongana majina ya filamu wakati visa tofauti inawezekana isiwe tatizo, labda itokee kuwa hata visa vilingane, ukija kwa upande mwingine lazima vyombo husika vilivyopo vijitahidi kuwa na kalenda ya kuwaongoza watayarishaji ikiwa na utaratibu wa kuzipitia script kabla ya kwenda kurekodi.
Tukio hili si kwanza kutokea lilishawahi kutokea kati ya mtayarishaji Mohamed Nurdin na Gumbo Kihorota, ambapo Gumbo alitoa filamu iliyoitwa Machozi na Mohamed Nurdin naye baadae akatoa filamu iliyoitwa Machozi vile vile, sikufuatilia huko mbele sina kumbukumbu kama kuna mmoja wao aliathirika na hilo.
Watayarishaji mjitahidi kubuni majina ya Kiswahili inawezeka kabisa utata wa kugombea majina ukapotea kwani Lugha yetu ina uwanda mpana na wenye maana tofauti, tofauti na Lugha tunayoikimbilia.
No comments:
Post a Comment