BLOGGER TEMPLATES AND TWITTER BACKGROUNDS »

Promo

Promo

Monday, May 28, 2012

Serikali yataka maombi ya uchunguzi wa umri wa Lulu yatupwe


UPANDE wa mashtaka katika kesi ya mauaji inayomkabili msanii wa filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu ambaye anakabiliwa na kesi ya mauaji ya msanii mwenzake Steven Kanumba umepinga maombi yaliyowasilishwa Mahakama Kuu kuhusu umri wa mshtakiwa huyo na kuiomba mahakama hiyo iyatupilie mbali.

Pingamizi hilo la awali liliwasilishwa mahakamani hapo jana na mawakili wa upande wa mashtaka Elizabeth Kaganda na Shadrack Kimaro mbele ya Jaji Dk Fauz Twaib wakati wa kusikilizwa maombi hayo.
Akiwasilisha pingamizi hilo, wakili Kimaro alidai kuwa maombi hayo yamewasilishwa mahakamani hapo kinyume cha sheria.

Alidai kuwa hata vifungu vya sheria namba 120 (ii) na 113 (i) na (ii) vya sheria ya mtoto ya mwaka 2009 ambavyo upande wa utetezi umevitumia kuwasilisha maombi hayo haviipi mamlaka mahakama hiyo kuweza kusikiliza maombi hayo.

“Namna walivyowasilisha maombi yao na sababu walizozitaja hazitoshi kuiruhusu mahakama hii kusikiliza maombi yao,”alidai Kimaro na kuongeza kuwa:

“Ni kweli kwamba mahakama hii ina uwezo wa kusikiliza suala la umri, lakini namna upande wa utetezi walivyowasilisha maombi yao hakuiwezeshi mahakama hii kuyasikiliza,”alidai.

Kimaro alidai kuwa mojawapo ya kielelezo kilichowasilishwa na upande wa utetezi wakidai ni uamuzi uliotolewa na mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu si uamuzi bali ni amri ya mahakama.
Akijibu hoja hizo, wakili wa utetezi Kenedy Fungamtama ambaye alikuwa akisadiana na Fulgence Massawe na Peter Kibatala, alidai kuwa maombi yao ni ya msingi kwani wamefuata taratibu zote za kisheria na kuomba mahakama iyasikilize.

“Tulichofanya tumefanya kwa kufuata amri iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kilichoko hapa ni ubishi kuhusiana na umri wa mshtakiwa,”alidai Fungamtama na kuongeza kuwa:

“Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haikutoa uamuzi bali ilitoa amri kwa mawakili wa mshtakiwa kama wana maombi yoyote wafanye hivyo kupitia mahakama kuu na ndivyo tulivyofanya,”alidai.

Wakili huyo wa utetezi aliendelea kudai kuwa, hata katika sheria ya mtoto ya mwaka 2009 imetafsiri neno mahakama ikimaanisha kuwa ni ile ya mwanzo, wilaya, mkoa ama mahakama kuu hivyo ni sahihi maombi yao kuwapo mahakamani hapo.

“Upande wa mashtaka wameshindwa kuisaidia mahakama hii ni taratibu zipi ambazo hatukuzifuata katika kuwasilisha maombi haya hivyo pingamizi lao litupiliwe mbali,”alidai Fungamtama.

Upande wa utetezi pia ulinukuu kesi mbalimbali zikiwamo rufaa ya madai namba 86/2009 kati ya Samson Mwalida na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na  kati ya Farida na Kampuni ya Scania Tanzania Ltd.

Jaji Twaibu baada ya kusikiliza hoja zote, aliwauliza maswali.Jaji: Je mnadhani Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haikuwa na mamlaka ya kusikiliza maombi haya?
Jaji: Nikiangalia kumbukumbu katika jalada hili wakili Kaganda (upande wa mashtaka) alisema Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza maombi haya kwasababu kesi iliyoko mbele yake ni ya mauaji ambayo husikilizwa na mahakama kuu.

Kaganda: Mtukufu Jaji mimi nilisema hivyo nikimaanisha kwamba bado tunaendelea na upelelezi na kati ya vitu tunavyochunguza ni pamoja na suala la umri wa mshtakiwa.
Baada ya kusikiliza hoja zote Jaji Twaib aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 11 mwaka huu atakapotoa uamuzi kuhusiana na maombi hayo.

Upande wa utetezi umewasilisha maombi hayo ukiiomba mahakama kuu iangalie na kuona kama mahakama ya kisutu ina uwezo wa kuamua suala hilo.

No comments:

Post a Comment