BLOGGER TEMPLATES AND TWITTER BACKGROUNDS »

Promo

Promo

Sunday, June 19, 2011

Majina ya Kiingereza Filamu za Kibongo ni Ushamba?


NI jambo la kufurahisha sana kuona kuwa hivi sasa tumekuwa tukijitahidi kujitutumua na kupiga hatua katika uandaaji wa filamu hapa nchini.
Si tu kuwa inafurahisha bali pia inatia moyo na kuleta fahari kwetu Watanzania kwani katika kipindi cha miongo mingi, tumeonekana kuwa nyuma katika fani mbalimbali za sanaa.
Chimbuko lililopo sasa la utitiri wa filamu hizi na zile za Kizalendo, linadhihirisha mbio za dhahiri shahiri zenye dhati ya kuelekea kilele cha mafanikio ya kweli katika soko la filamu.
Lakini licha ya mbio hizo, kuna jambo moja ambalo kwakweli ni kero kwa mashabiki na wapenzi wa filamu hizo za Kibongo kwa ujumla ambazo zimezalishwa na waandaaji, wasambazaji pamoja na wazawa ambao ni Watanzania wenyewe.
Nalo si jingine bali ni hii desturi ya filamu nyingi, kama si zote zinazofyatuliwa sasa kuwa na majina ya Kiingereza huku yanayoonekana ndani yameigizwa katika mazingira pamoja na lugha ya Kiswahili.
Binafsi nimekuwa nikijiuliza mara nyingi tatizo ni nini? Ni ulimbukeni wa Lugha, kudharau lugha yetu ya Kiswahili inayokua kwa kasi au nini?
Labda pengine mnaiga kutoka katika mataifa Fulani, lakini kama ndivyo, mtakuwa mnakosea sana, kwa sababu kila taifa lina mila, desturi na utamaduni wake katika masuala mbalimbali, hasa ya burudani ambayo ni sehemu ya kielelezo cha taifa.
Kutokana na hali hiyo, hata wanunuzi wa nje wanaponunua na kukuta kilichoandikwa nje si kilichomo ndani, wengi wamekuwa wakitushusha Watanzania wote.
Hivyo kwa ushauri wa bure kwa wasanii wetu, wawe makini na majina ya Kiingereza wanayoyanadi katika makasha yaende sambamba na hadithi husika, vinginevyo tutabaki kuwa malimbukeni wa lugha za watu.
Mbona hapo awali katika michezo ya kuigiza, tamthilia pamoja na filamu za waliowatangulia hakukuwahi kutokea kitu kama hicho wa kuidhihaki lugha yetu na walisikika na kuvutia, hata sasa tunawakosa sana.
Kwa kuthibitisha hilo, hata sasa tunashuhudia wasanii wakongwe wengine waliosalia kama vile Said Ngamba ‘Mzee Small’ na Amri Athuman ‘King Majuto’ wanavyoendelea kukienzi Kiswahili chetu ambapo katika filamu na tamthilia zao zote mwendo ni wa kizalendo pekee.
Nawauliza wasanii wetu wa kizazi kipya kwanini msiige kutoka kwao? Au ndiyo mnaendekeza ile dhana ya kuwa wamepitwa na wakati na wenye mawazo yaliyokwishakuwa ya kizamani! Fahamuni kuwa mnapotea kwa kuelekea mahali ambako siko tunakokuhitaji.
Nikiwa mdau wa burudani, nachukua fursa hii kuviomba vyama pamoja na mabaraza yanayohusika na usimamiaji wa masuala ya filamu, kulitazama hili kwa macho makini ili kuepuka athari kubwa inayoweza kutokea hapo baadaye.
Pia nawaomba wahusika wenyewe ambao ni watayarishaji pamoja na waigizaji kuhakikisha wanakienzi Kiswahili chetu kwa kuachana na ulimbukeni wa kutoa filamu zenye majina ya Kiingereza.


No comments:

Post a Comment