MSANII nyota wa bongo movies Bakari Makuka (Beka), amesema ataanza kucheza tamthilia ili kuibua vipaji vya wasanii wengi wenye maadili na kuwa nyakati hizi wasanii wakongwe wametosa mchezo huo.
Beka ambaye anaelekeza hisia zake katika kuiteka tasnia hiyo alijizolea sifa lukiki miaka ya 2002 alipokuwa katika kundi la Nyota Academia lililokuwa linaongozwa na msanii nguli wa filamu Singo Mtambalike (Richie).
Anasema, tamthilia zilizokuwa zinachezwa na wasanii kipindi hicho ziliweza kuwapatia wasanii mafunzo na maadili mazuri lakini sasa wasanii hao wanawatumia watu ambao hawana maadili katika kazi hiyo kwa lengo la kuuza kazi na sio kuipatia jamii ujumbe husika.
“Binafsi nimeanza kuzalisha filamu zangu lakini nitajikita zaidi kwenye tamthilia kwa sababu kwa sasa zimeachwa sana na ndio maana maadili ya sanaa hayafuatwi,” anasema.
Beka anaongeza kuwa, “Tulipokuwa kwenye vikundi vya maigizo (tamthilia) tulikuwa tunafundishwa maadili ya kazi na wasanii walioko kwenye gemu sasa hivi na waliopitia vikundi wanatambua, tatizo ni moja tu wasanii wakubwa hawawatumii watu wenye taaluma wanatoa kazi kwa mto ilimradi auuze tu,”.
Alisema, tamthilia zinazotakiwa kuchezwa zinatakiwa kubeba uhusika wa jambo na muwakilishi anapaswa kuuvaa uhalisia ili jamii iweze kupata ujumbe uliotarajiwa.
Beka anasema, tamthilia za aina hiyo zitafanikisha katika kuendana na ushindani wa soko la sanaa na kuwa wasanii kama Bi Kikokwa, Bi Mkora na wengine waliotikisa enzi hizo ni mfano wa kuigwa.
Anasema, katika kuwapata wasanii watakaocheza tamthilia hizo atatumia mfumo wa kupiga kura kwa kila jina litakalopendekezwa ili kazi iweze kufanikiwa zaidi.
“Nataka kuwa tofauti na wasanii wengine sitafurahia pale kazi yangu itakapopokelewa tofauti na jamii, cha msingi nitatumia mfumo wa kupiga kura kwa kila mtu ambaye atapendekezwa sio kuhonga lengo langu ni kurudisha hadhi ya tasnia ya filamu katika mstari wake,” anasema.
Aidha, Beka anasema tayari ameaanza kucheza filamu zake mwenyewe mbili na kuwa moja inaitwa I hate my wife ambayo imetengenezwa na kampuni ya Msekwa Media.
No comments:
Post a Comment