MSANII machachari wa filamu nchini Yusuph Mlela ameamua kuvunja ukimya baada ya kudai kuwa wazalishaji wa filamu (Producer) wanashusha viwango vya utendaji kazi wa wasanii.
Mlela anasema asilimia kubwa ya wazalishaji hao wamekosa uaminifu katika kazi hiyo hali ambayo ni kinyume na maadili ya kazi na inayokatisha tamaa kwa wasanii.
“Sanaa yetu inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya maproducer kushindwa kuwalipa wasanii fedha zao kwa muda, unaweza kucheza filamu ukamaliza lakini usilipwe fedha halali uliyokuwa umeahidiwa, hili ni tatizo,” anasema.
Anasema, wazalishaji wanatakiwa kuwa waaminifu ili tasnia ya filamu iweze kukua na kutoa motisha kwa wasanii utakaosaidia kuwafanya waipende kazi na kubadilisha mfumo mzima wa sanaa nchini.
“Gemu ya sanaa imekuwa sana hata soko limekuwa kiasi ingawa bado unyonyaji upo, hatuna hatimiliki na ndio maana hata kazi zetu hazitoki nje ya Tanzania,”anasema.
Anasema, serikali inatakiwa kuingilia kazi za wasanii ili kusaidia kulinda faida yao na kwamba sanaa inaajiri vijana wengi.
Akizungumzia mafanikio yake Mlela anasema, amefanikiwa kumiliki kampuni yake mwenyewe (Mlela Production) itakayoshughulika na masuala ya picha na matangazo.
“Kampuni ndio imeanza kufanya kazi hivi karibuni, tumeanza kushuti filamu itakayotambulika kwa jina la Mayenzo, imechezwa na Hemed Suleiman, Slimu, Nishi na mimi mwenyewe,”anasema.
No comments:
Post a Comment